Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal ameihakikishia Taasisi ya kusaidia kuhifadhi wanyamapori Tanzania kuwa serikali itafanya kila jitihada ili kulinda wanyamapaori nchini. Akizungumza katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Taasisi hiyo katika hotel ya Moven Pick jijini Dar es salaam jana Dk. Bilal alisema hatua hiyo ya serikali inatokana na ukweli kwamba uhai wa wanayamapori ni suala linalohusu watu wote katika jamii. Alisema serikali itaanza mpango mkubwa na wa muda mrefu wa kupambana na majangiri katika Hifadhi za Taifa na mbuga za wanyama na itakapobidi serikali iko tayari kutumia mbinu zote zilizopo kufanya operesheni maalum kulinda wanyamapori katika hifadhi hizo. Alisema serikali pia inatarajia kutumia teknolojia ya kisasa katika kukabiliana na majangiri na hali kadhalika kutunga sheria kali ambazo zitakuwa na faini kubwa na pia kifungo cha muda mrefu kwa watu watakaobainika kuwa majangiri. Makamu wa Rais alibainisha wazi kuwa tangu Taasisi hiyo ikutane kwa mara ya mwisho mwaka 2008 hifadhi za wanyamapori zimekuwa hatarini kwa kuwa kiwango cha vitendo vya uhalifu kimeongezeka na kusema tabia hiyo ya uhalifu haikubaliki kwani mbali ya kuhatarisha usalama wa wanyamapori lakini pia inatishia biashara ya utalii. “Baadhi ya watafiti mashuhuri duniani wamekisia kuwa kiwango cha sasa cha ujangiri katika mbuga za wanyama, iwapo tembo hawatalindwa dhidi ya majangiri wanaweza kupotea ndani ya miaka 10 ijayo. Kwa kweli hali hii inatukumbusha kazi kubwa iliyoko kwetu sote sisi,” alisema Makamu wa Rais. Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige alielezea changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya ujangiri katika maeneo ya hifadhi, upungufu wa magari na watumishi. Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo J.K. Chande pamoja na kusisitiza serikali iweke sheria kali ya kuzuia majangiri pia alieleza kuwa Taasisi hiyo imefanikiwa kupata magari 15 aina ya Land Cruiser tangu ianzishwe mwaka 2001 kwa ajili ya kusaidia watumishi kuendesha shughuli zao. Naye Mwakilishi wa Mtoto wa Mfalme wa Austria ambaye ni mweka hazina wa Taasisi hiyo Jacques Servais aliipongeza Taasisi ya kusaidia kuhifadhi wanyapori Tanzania kwa kufanikisha shughuli zake vyema tangu ilipozinduliwa mwaka 2001. Hafla hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kukusanya fedha ilihudhuriwa pia na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ambaye ni mlezi wa Taasisi hiyo pamoja na mkewe Mama Anna Mkapa. Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Dar es salaam Jumapili – April 16, 2011 |
Sunday, 1 May 2011
Serikali kulinda wanyamapori – Dk. Bilal
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment