Saturday 21 May 2011

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL MGENI RASMI MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA WAUGUZI MNAZI MMOJA DAR


  • Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akimkabidhi zawadi, Paul King’ara Muuguzi kutoka mkoani Mwanza wakati wa maadhimisho ya Sherehe za ya miaka 40 ya kuzaliwa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), zilizofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salam leo Mei 20.
  • Wauguzi fuateni maadili ya kazi zenu – Dk. Bilal
    Na Mwandishi Maalum – Dar es salaam
    Ijumaa – Mei 20, 2011
     
    Serikali imewataka wauguzi na wakunga nchini kufuata maadili na miiko ya kazi zao katika kuwahudumia wagonjwa.
    Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha siku ya wauguzi na wakunga duniani Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amesema kazi za wauguzi na wakunga huonekana kwa ukaribu zaidi na ni rahisi kwa wateja kuwafanyia tathmini.
    “Pale mnapofanya kazi zenu vema, sisi tunafarijika sana. Na pale mnapoenda kinyume na miiko ya kazi yenu, jamii husikitika sana. Kumbukeni kuwa jukumu lenu kwa wananchi ni zito na tena mnapaswa kulibeba jukumu hilo kwa moyo wa ustahimilivu,” alisema Makamu wa Rais.
    Katika sherehe hizo ambazo zimefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya Chama cha Wauguzi nchini  (TANNA) Dk. Bilal aliwakumbusha wauguzi umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri na wagonjwa.
    Alisema serikali inatambua changamoto zinazowakabili wauguzi na kusema imekuwa ikijitahidi kwa kadri hali ya uwezo wa uchumi inavyoruhusu kusaidia kuboresha sekta ya afya nchini.
    Alibainisha kuwa serikali imejitahidi kuongeza idadi ya wanafunzi katika vyuo nchini wanaosomea uuguzi na pia imekuwa ikiwatumia madaktari kutoa semina kwa wakunga hasa waliopo vijijini kwa lengo la kuboresha huduma hizo kwa wananchi.
    “Tunatambua kuwa bado suala la upungufu wa wauguzi ni kubwa na tena tunaelewa kuwa tatizo la uhaba wa vifaa vya kazi katika sekta ya afya limekuwa likiongezeka,” alisema Makamu wa Rais na kuongeza
    “Yote haya wakati sisi tunayafanyia kazi kwa upande wetu na nyie kwa upande wenu fanyeni vema katika yale yaliyomo ndani ya nafasi zenu, mfano ni huu wa kujenga mahusiano mazuri na wagonjwa kila wanapohitaji huduma kutoka kwenu.”    
    Akizungumza katika sherehe hizo Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Bibi Romana Sanga aliiomba serikali kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wauguzi hali ambayo itachangia kuwawezesha wauguzi kuwahudumia wagonjwa kwa ufanisi. Sherehe hizo zilianza kwa maandamano  ya wauguzi na wakunga kutoka kote nchini ambayo yalipokelewa na mgeni rasmi Dk. Bilal

No comments:

Post a Comment