Tuesday 14 June 2011

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AKUTANA NA WATANZANIA WAISHIO NEW YORK, ASISITIZA KUZINGATIA MAONI KUHUSU KATIBA.











Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Watanzania waishio New York na Vitongoji vyake, wakati alipokutana nao kwa ajili ya mazungumzo jana Juni 12, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR



TUTAZINGATIA MAONI NA USHAURI KUHUSU KATIBA-DKT. BILAL

Na Mwandishi Maalum, New York
SERIKALI imesisitiza nia yake ya kuhakikisha kwamba zoezi la kukusanya maoni, ushauri na mapendekezo kuhusu mchakato wa  kutungwa kwa Katiba mpya linafanyika kwa  uwazi na umakini mkubwa.
 Hayo yameelezwa na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Ghalib Bilal wakati alipokuwa akisalimiana na watanzania wanaoishi katika jiji la New York na vitongoji  vyake.
Katika mazungumzo yake na watanzania hao yaliyofanyika  siku ya jumapili katika Makazi ya Balozi wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa, Makamu wa Rais amesema,  ni dhamira ya serikali kuhakikisha si tu inawapa wananchi fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo, lakini kila hoja itakayotolewa itazingatiwa kwa kadri ya  uzito wake.
“ Tumeanza zoezi hili,  ni zoezi ngumu lakini  ni zoezi muhimu sana katika kukuza na kudumisha demokrasia yetu. Ni zoezi ambalo linavuta hisia za watu wengi na linafuatiliwa kwa makini sana na wadau mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje.” Akasema Makamu wa Rais.
Na kuongeza kuwa  mchakato huo pia unafuatiliwa  na majirani zetu ndani ya Jumuia ya Afrika  Mashariki  (EAC)na Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC). “ Kinachofanyika hivi sasa nchini Tanzania  kinakuwa na rasharasha katika sehemu mbalimbali, wanafuatilia kuona nini kitatokea na hii ni ishara nzuri” akasisitiza.
Akasema kuwa  hamu ya wadau hao kuufuatilia mchakato huo,  inatokana na sababu nyingi lakini kubwa ni kuwa Tanzania bado ni nchi nzuri na inayozingatia   utawala wa kidemokrasia.
Akijibu maswali na hoja mbalimbali zilizotolewa na watanzania hao. Yakiwamo maswali kuhusu matatizo ya umeme, mfumuko wa bei hasa kwenye mafuta,  uraia wa nchi mbili na fursa za kupata  ajira nchini Tanzania.
Katika kuelezea tatizo la umeme, Dkt. Bilal alikiri kuwapo kwa tatizo  hilo, na akaainisha hatua ambazo serikali imechukua kukabiliana nalo, baadhi  ya hatua hizo ni pamoja na  kutafuta vyanzo vingine vya umeme kama vile umeme wa  upepo, umeme wa gesi asilia na umeme utakao tokana na makaa ya mawe.
Akasema  matatizo hayo ya umeme yamekuwa na athari nyingi katika utendaji kazi na ukuaji wa uchumi. Aidha ameeleza kuwa tatizo la umeme linachangiwa na mambo mengi kama vile upungufu wa mvua na uongezeko la matumizi ya nishati hiyo.
Kuhusu bei ya mafuta, Makamu wa Rais alisema kupanda kwa bei ya mafuta   ni tatizo la dunia nzima. Hata hivyo akasema kuwa kuna chombo ambacho kimepewa kazi ya kudhibiti bei ya mafuta na  ubora wake.
Akasema chombo hicho (EWURA) kina mamlaka yote,  tena kiko huru na hakiingiliwi na mtu yeyote.  Hadi sasa kinafanya kazi nzuri. Lakini kinauwezo wa kufanya  kazi nzuri zaidi kwa kuwa hakiingiliwi na serikali  na akaeleza kuwa atashangaa sana kama chombo hicho kitashindwa kutekeleza majukumu.
Kuhusu hali ya chakula, Makamu wa  Rais alisema kuwa baadhi ya maeneo ya nchi yatakuwa na upungufu mkubwa  hasa kwa zao la mpuga kutokana na uhaba wa mvua. Hata hivyo akasema serikali imejiwekea mipango madhubuti ya kuhakikisha kuwa wananchi watakaopungukiwa   chakula wanapata chakula kutoka hifadhi ya taifa.
Wakati huo huo, Waziri wa Afya  kutoka Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, Mhe. Juma Duni Haji amewataka watanzania wanaoishi ughaibuni kuacha kulalamika na kulaumu.
Alikuwa akichangia kujibu maswali  kuhusu nini serikali inafanya katika uboreshaji wahuduma za afya .
 “ Serikali inafanya lile linalowezeka na kila jambo linafanywa  kwa wakati wake na kwa kipaumbele chake, matatizo ni mengi na hayawezi kutatuliwa yote kwa wakati mmoja. Lakini nitoe rai yangu, acheni kulalamika na kulaumu, muda wa kulalamika na kulaumiana umeshapita. Kinachotakiwa ni kushirikiana sote katika kujenga nchi yetu” akasisitiza Waziri wa Afya.

No comments:

Post a Comment