Tuesday 21 September 2010

Wapuuzeni wanaodharau sekondari za kata

Na Mwandishi Wetu,Tabora

MGOMBEA Mwenza wa nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Mohamed Gharib Bilal amewataka wananchi wa mkoa wa Tabora kuwapuuza wanaotoa kauli za bezo dhidi ya mpango wa serikali kujenga shule za sekondari za kata.
 Kauli hiyo ya Mgombea Mwenza huyo, aliyepo katika mikutano ya kampeni katika mikoa ya Kati, aliitoa jana katika mji wa Tabora, ambapo pia alipata fursa ya kuwahutubia mamia ya wananchi waliofurika katika uwanja wa sekondari ya Uyui.
 “Nawaambieni wapuuzeni sana hawa wapinzani wanaotoa kauli tamu tamu ambazo hazitekelezeki. Nawaambieni wana Tabora kuwa hawafai kuchaguliwa na msiwape kura. Haiwezekani kabisa kwa mtu anayetambua maendeleo ya elimu nchini atoe kauli za bezo dhidi ya ujenzi wa shule za sekondari za kata kwa kuziita shule za ‘Yebo Yebo’,” alisema na kuongeza;
 “Asilimia zaidi ya 50 ya wanafunzi wanaofaulu na kuingia vyuo vikuu kwa sasa wanatoka katika shule za kata. Wote hawa wanapatikana baada ya mpango mzuri wa serikali ya CCM kuamua kujenga shule hizi. Kama shule hizi hazingekuwepo vijana hawa wangekuwa wapi?” alihoji huku umati mkubwa ukimshangilia na kumtaka aendelee kuzungumza.
 Dk Bilal ameingia katika mkoa wa Tabora akitokea visiwani Zanzibar ambako huko alipata fursa ya kuhudhuria mikutano ya kampeni za CCM zilizokuwa na lengo la kuzindua kampeni za CCM sambamba na kumtangaza rasmi kwa wananchi  mgombea urais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein.Kabla ya kwenda Zanzibar, Dk Bilal alikuwa mkoani Singida na msafara wake uliungana naye jana mkoani Tabora ambapo alipata pia fursa kufanya mikutano ya kampeni katika wilaya za Igunga na Nzega. Akiwa wilayani Igunga, mgombea mwenza huyo alipata fursa ya kumnadi mgombea ubunge wa CCM Rostam Aziz na akawataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua kwa kura nyingi kwa kuwa wanafahamu mambo mbalimbali anayowafanyia katika jimbo hilo.Akiwa katika kijiji cha Ndalla katika wilaya ya Nzega, mgombea huyo pia alimnadi mgombea wa CCM, Dk Hamis Kigwangala huku akisisitiza umuhimu wa wananchi wa jimbo hilo hasa wapenzi wa CCM kuungana katika kipindi hiki cha uchaguzi ili kukihakikishia chama chao ushindi.Leo mgombea Mwenza huyo anakamilisha mikutano yake ya kampeni katika wilaya ya Urambo na kisha anatarajiwa kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya kuendelea na mikutano ya kampeni.

No comments:

Post a Comment